Mwanamuziki nguli wa nyimbo za mtindo wa Afro Jazz kutoka Kenya Achieng Abura amefariki dunia.
Mwanamuziki huyo aliaga dunia akipokea matibabu katika hospitali kuu ya taifa ya Kenyatta (KNH) jijini Nairobi.
Lydia Achieng Abura, alipata umaarufu miaka ya 1990 kwa wimbo wa injili kwa jina I Believe.
Baadaye, alianza kukumbatia mitindo mingine ya uimbaji kama vile jazz.
Kwenye ujumbe katika ukurasa wa Facebook mapema mwezi huu, alikuwa amedokeza kwamba hakuwa buheri wa afya.
Alisema alikuwa amepoteza uzani wa kilo 50 katika kipindi cha miaka mitatu pekee, na madaktari walikuwa wamemshauri kuongeza uzani.
"Kutembea ni shida na ninaumwa kila pahali," aliandika.
Kwenye mahojiano na gazeti la Business Daily mwezi Julai, alikuwa amesema alikabiliwa na matatizo ya kifedha kutokana na afya ya mwanawe wa kiume aliyehitaji kufanyiwa matibabu ambayo yangegharimu Sh4 milioni (dola 400,000 za Marekani).
"Niliandaa mchango lakini waliohudhuria walikuwa chini ya 10," aliambia gazeti hilo.
Abura alishinda tuzo ya muziki ya Kora mwaka 2004.
Alikuwa pia jaji katika shindano la kuwatafuta wanamuziki wenye vipaji la Tusker Project Fame ambalo liliwashirikisha vijana kutoka nchi za Afrika Mashariki.
Wanamuziki wenzake, viongozi na mashabiki wameeleza kushangazwa kwao na kifo hicho na wamekuwa wakituma salamu za rambirambi mtandaoni.