Mwinjilisti wa Kanisa la African Inland Church (AICT), Charles Kazereng’wa (45), amejinyonga hadi kufa, baada ya kumuua mwanaye, Malita Charles (15) kwa kumpiga akimtuhumu kujihusisha na ufuska
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Mponjoli Rodson amelithibitishia gazeti hili kutokea kwa matukio hayo juzi jioni.
Hata hivyo, alisema kuwa asingeweza kulizungumzia suala hilo kwa undani kwa sababu alikuwa kwenye sherehe za uzinduzi wa Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani ambayo kitaifa inafanyika mkoani Geita.
Hata hivyo, habari za uhakika kutoka katika Kitongoji cha Elimu, Kijiji cha Kaseme kilichopo wilayani Geita ambako mwinjilisti huyo alikuwa akiishi na familia yake zinasema kuwa alichukua uamuzi wa kumwadhibu binti yake huyo aliyehitimu darasa la saba mwaka huu, baada ya kumkuta akizungumza na mwanamume ambaye hata hivyo hakufahamika.
Inaelezwa kuwa baada ya kumpiga, alimchukua na kwenda naye nyumbani na kumfungia ndani huku akiendelea kumwadhibu hadi alipofikwa na umauti.
Kwa mujibu wa shuhuda ambaye hakuwa tayari kutajwa jina gazetini, baada ya mwinjilisti huyo kubaini kuwa amemuua mwanaye, alichukua uamuzi wa kukimbia umbali ya kilometa moja na kujitundika mtini kwa kamba iliyomnyonga hadi kufa.
Kamanda Mponjoli, alisema kuwa uchunguzi wa Polisi na wa madaktari unaendelea na kwamba utakapokamilika miili ya marehemu wote wawili itakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko.
Aliitaka jamii kuwa makini wakati wa kuadhibu watoto kwa kuwa si wakati wote wanapaswa kupewa adhabu kali na hatarishi kama vipigo vinavyoweza kuwasababishia umauti.
Wakati huohuo, baadhi ya wakazi wa Kata ya Kaseme wanaomfahamu mwinjilisti huyo walieleza kwa nyakati tofauti kushangazwa na hatua aliyoichukua kwa sababu hakuwa na tabia ya uhalifu wa aina yoyote wala ukatili.
Masaga Makanika na Magesa Masai kila mmoja kwa wakati wake alisema kuwa mwinjilisti huyo alikuwa ni muumini mzuri wa dini asiye na rekodi mbaya ya matukio ya kiuhalifu na kwamba hatua alizochukua zimewaacha na maswali mengi huku wakifikiri kuwa pengine ni mipango ya Mungu au majaribu ya shetani.
Source: Habari Leo
Source: Habari Leo