Thursday, July 14, 2016

JESHI LA UGANDA LAINGIA SUDAN KUSINI

Msafara wa wanajeshi wa Uganda waliojihami umeingia Sudan Kusini kufuatia amri ya rais Yoweri Museveni kwenda kuwanusuru waganda walioathirika katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe juma lililopita.
Msafara huo wa malori 50 ya kijeshi yanapewa usalama na vifaru vidogo vya jeshi la UPDF.
Madafara huo uliingia ardhi ya Sudan Kusini kupitia kivuko cha Nimule takriban kilomita 200 kutoka Juba na unatarajiwa kuelekea hadi mji huo mkuu kuwanusuru waganda walioko huko.
''Tunaenda Juba kuwanusuru takriban waganda 3,000 ambao wamekwama huko kutokana na machafuko yaliyotokea juma lililopita kati ya wanajeshi watiifu kwa rais Salva Kiir na wale watiifu kwa Makamu wake bwana Riek Machar.''
Brigadier Leopold Kyanda ameiambia shirika la habari la AFP kuwa ''hatutasita kuwasaidia wale wanaotaka kuondoka awe ni Mganda ama hata raia wa Sudan Kusini yenyewe''
''Bila shaka idadi hiyo inaweza kupanda zaidi''
Rais Yoweri Museveni alikuwa ametoa agizo kwa jeshi la taifa UPDF kwenda Sudan Kusini kuwaokoa raia wake walioko huko.
Msemaji wa jeshi Paddy Ankunda amenukuliwa akithibitisha kuwa kikosi kidogo cha wanajeshi kitakwenda kwa barabara kuwaokoa waganda walioathirika na mapigano


Hatua hiyo ilifuatia ripoti ya mauaji ya wafanya biashara watano raia wa Uganda miongoni mwa watu zaidi ya 272 waliouawa majeshi watiifu kwa rais Salva Kiir walipokabiliana vikali na wanajeshi watiifu kwa makamu wa rais wa Sudan Kusini bw Riek Machar mjini Juba.
Mashirika ya misaada yanasema hakuna maji safi ya kunywa na mahitaji muhimu.
Mji wa Juba hutegemea maji yanayosambazwa kwa matrela kwani hakuna mabomba ya maji.
Umoja wa mataifa unasema karibu watu elfu 40 wamekimbia mapigano ya karibuni, lakini huenda idadi hiyo ikawa kubwa zaidi.
Kwa sasa mustakabali wa taifa hili changa zaidi la Afrika haujulikani, matumaini yakiwa katika kutekelezwa kwa mkataba wa amani wa mwaka uliopita.

No comments:

Post a Comment