CHINI ya kocha Joseph Omog kikosi cha Simba sasa kitaingia kambini
mjini Morogoro kujiimarisha zaidi kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu
Tanzania Bara.
Omog ambaye amemwaga wino wiki iliyopita kukinoa kikosi hicho cha
Msimbazi na tayari mapema wiki hii, ameanza mchakamchaka kwa wachezaji
wake katika Uwanja wa Bandari Kurasini.
Omog amekuwa akitumia muda mwingi kuwapa mazoezi ya kukimbia uwanja
kwa saa tatu pamoja na mazoezi ya viungo, lengo likiwa ni kuwatengenezea
stamina na pumzi ili wamudu kucheza dakika 90 uwanjani. “Nimewapa
mazoezi ya kuongeza stamina, nguvu na pumzi ili wachezaji wangu wamudu
kucheza mpira.
“Nimefikia hatua hii baada ya kuwaona wachezaji wanachoka mapema
baada ya kuwapa mazoezi ya kukimbia mbio ndefu na fupi, ninataka timu
imudu kucheza dakika zaidi ya 90 katika mechi,” alisema Omog ambaye
ameapa msimu ujao Simba inapanda ndege kushiriki michuano ya kimataifa
kwani atahakikisha Wekundu hao wa Msimbazi wanamaliza ukame wa mataji.
Alisema ana mifumo mingi mpaka sasa hajajua atumie mfumo upi ambao
utaendana na kikosi chake ambacho amekiri hajawafahamu vizuri wachezaji
wake na kwamba atakapokaa nao angalau kwa wiki mbili zaidi atajua ni
mfumo upi sahihi wa kwenda nao kutokana na aina ya wachezaji wake.
Kikosi hicho kitajichimbia Morogoro kwa muda wa wiki mbili kabla ya
kuvuka maji kuweka kambi Zanzibar kwa muda wa wiki mbili ikijiandaa na
Ligi Kuu Tanzania bara inayotarajiwa kutimua vumbi Agosti 20 mwaka huu.
Hata hivyo, kabla ya mchakamchaka wa ligi timu hiyo itacheza mchezo
wa kirafiki na Gor Mahia kwenye tamasha la Simba Day litakalofanyika
Agosti 8 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Rais wa Simba, Evans Aveva amekaririwa akisema wachezaji wote
waliosajiliwa na timu hiyo watakwenda kambini Morogoro kwa ajili ya
kuanza kujifua wakiwa chini ya Kocha Mkuu mpya Mcameroon Joseph Marius
Omog ambaye aliwasili nchini wiki iliyopita na kurithi mikoba ya
Muingereza Dylan Kerr, aliyefukuzwa Januari.
Aveva alisema lengo la kuandaa kikosi chao ni kuhakikisha msimu ujao
wanafanya vizuri na kuondoa ukame wa vikombe unaokabili klabu hiyo kwa
miaka minne mfululizo na kuwapa raha mashabiki na wanachama wao.
No comments:
Post a Comment