Thursday, July 14, 2016

SAKATA LA JERRY MURO LACHUKUA SURA MPYA.

SAKATA la msemaji wa Yanga, Jerry Muro na uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limechukua sura mpya baada ya kutakiwa kuwa na adabu, kwani adabu hainunuliwi dukani.

Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa alisema kwa kifupi, “Adabu hainunuliwi Cairo”.
Kwa upande wa Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alionesha kushangazwa na kauli kali zinazoendelea kutolewa na Muro, hata hivyo alidai kuwa kwa upande wa TFF walishafunga mjadala wa suala hilo.
“Hukumu ilishatoka, alishapewa nakala ya hukumu yake, yeye kama anaendelea kutoa lugha za kukashifu, muache aendelee sisi kwa upande wa TFF tulishalifunga suala hilo,” alisema Lucas.
Kauli ya viongozi hao wa TFF imekuja ikiwa ni saa chache baada ya Muro kudai kuwa ana akili nyingi kuliko viongozi wa TFF na kutaka wasimsumbue kwani yeye sio mwanachama wa TFF bali ni muajiriwa na wakiendelea kufanya hivyo atawaburuza kwenye mahakama za kawaida za kiraia.

Muro alienda mbali zaidi na kuhoji elimu ya viongozi hao wa soka. Hata hivyo, pamoja na Muro kudai kuwa yeye ni muajiriwa na si mwanachama wa TFF, Yanga ni mwanachama wa Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), CAF, FIFA na TFF, yeyote kiongozi wa Yanga anaweza kuadhibiwa na mashirikisho hayo kwa kuwa msemaji wa klabu ni agizo la Fifa ambalo lipo ndani ya katiba za wanachama wake na wanachama wa shirikisho husika.
Kwa mujibu wa kanuni ya 35 za soka za TFF inayozungumzia udhibiti wa viongozi, inasema kiongozi akitoa matamshi au ishara za matusi dhidi ya mashabiki, kwa nia ya kumdhalilisha kiongozi mbele ya jamii awe wa TFF, Klabu au Taifa atatozwa faini ya Sh milioni moja (1,000,000/-) na/ au kufungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi sita (6) au vyote kwa pamoja.
(i) Ni marufuku kwa kiongozi wa Kilabu kushutumu au kutoa matamshi yenye lengo la kumkashifu au kumdhalilisha kiongozi wa TFF/Chama cha Mpira cha ngazi husika kwenye vyombo vya habari.
(j) Hairuhusiwi kwa kiongozi au klabu kutoa matamshi au kuzungumzia jambo lolote linalohusu TFF kwenye vyombo vya habari bila ya kuwasiliana. (m) Pamoja na adhabu zilizoainishwa kwenye Kanuni hii TFF inaweza kutoa adhabu nyingine kwa kuongeza au kupunguza ikiona kuna ulazima.

No comments:

Post a Comment