TIMU
ya Vijana ya Kenya, imefuta ziara yake ya kwenda Dar es Salaam kwa
ajili kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya vijana wa
Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti
Boys.
Mchezo huo ulipangwa kufanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Julai 23, 2016.
Kwa
mujibu wa barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Kenya (FKF), Robert Muthomi kwenda Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), kufuta kwa ziara hiyo kunatokana na nafasi ambayo Kenya
imeipata.
Timu
ya Taifa ya Vijana ya Kenya imeteuliwa kushiriki michuano ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu la COSAFA inayotarajiwa kuanza Julai 22, 2016 hadi
Julai 31, 2016 mara baada ya Msumbiji kujitoa kwenye mashindano hayo.
“Tunaomba
kukutarifu kuwa timu yetu imetuliwa katika michuano ya vijana ya
COSAFA, hivyo ziara yetu Tanzania haitakuwako kama ambavyo sisi wenyewe
tuliomba mchezo huo kwenu (TFF) ufanyike Julai 23, 2016,” ilisema sehemu
ya barua hiyo iliyosainiwa na Muthomi.
Licha
ya kwamba mchezo huo hautakuwako, ratiba ya Serengeti Boys ambayo
inapambana kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Mataifa Afrika hapo
mwakani, imebaki vilevile kwa timu kuingia kambini Jumapili Julai 17,
2016 kwenye Hosteli za TFF zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume,
Ilala jijini Dar es Salaam.
Timu
hiyo inayonolewa na Bakari Shime itapiga kambi ya wiki moja katika
hosteli hizo, kabla ya kwenda Madagascar ambako itapiga kambi ya
takribani wiki mbili ikiwa ni ahadi ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi ambaye
alitoa ofa hiyo baada ya kuwatoa Shelisheli kwa jumla ya mabao 9-0
katika mechi zake mbili za kimataifa.
Serengeti
Boys inatarajiwa kucheza na Afrika Kusini kati ya Agosti 5, 6 au 7,
2016 huko Afrika Kusini kabla ya mchezo wa marudiano utakaofanyika saa
9.00 alasiri, Agosti 14, 2016 kwenye Uwanja wa Azam Complex, ulioko
Chamazi, Dar es Salaam.
Mshindi wa jumla katika michezo hiyo, itacheza na timu mshindi kati ya Namibia na Congo-Brazaville.
No comments:
Post a Comment