WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba amewasimamisha
kazi wakurugenzi watano wa idara tofauti katika wizara hiyo kutokana na
kuonesha udhaifu mbalimbali katika utendaji wao na wengine kusababisha
hasara katika usalama wa chakula.
Waliosimamishwa kazi ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa
Chakula nchini, Ombaeli Lemweli kutokana na kutoa vibali vya ununuzi wa
mazao na kuuzwa nje ya nchi ilhali tathmini ikiwa haijafanyika. Nafasi
yake kuchukuliwa na Elimpaa Kiranga aliyekuwa Mkurugenzi wa Bodi ya
Mazao Mchanganyiko.
Aidha, ameagiza kusimamishwa kazi kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Charles Walwa na nafasi yake
kushikwa na Deusdedit Mpazi aliyekuwa Meneja wa NFRA kanda ya Dodoma,
kutokana na kuharibu ghala la chakula na kusababisha hasara.
Viongozi wengine wa NFRA waliosimamishwa ni Mkurugenzi wa Uendeshaji
wa Huduma, Anna Ngoo, Mkurugenzi wa Masoko, Mikalu Mapunda na Meneja wa
NFRA, Songea Jeremia Mtafya ambao wametakiwa kupisha na uchunguzi
kufanyika mara moja dhidi yao.
Kadhalika, Dk Tizeba amemsimamisha kazi aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa
Mamlaka ya Bahari Kuu, Rashid Hoza na nafasi yake kushikwa na Hosea
Mbilinyi aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, lengo likiwa ni
kuimarisha ulinzi wa Bahari Kuu.
Mbali na nafasi hizo, pia Mkuu wa Kituo cha Utafiti cha Uyole mkoani
Mbeya, Dk Zakaria Maly amevuliwa madaraka na kuhamishiwa katika Kituo
cha Utafiti Seliani mkoani Arusha kuendelea na utafiti na badala yake
nafasi yake itachukuliwa na Arnold Msongi anayetoka Kituo cha Utafiti
Ilonga, Kilosa mkoani Morogoro.
Dk Tizeba alitoa maamuzi hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumzia
masuala mbalimbali, ikiwa ni mwezi mmoja baada yakuteuliwa na Rais John
Magufuli kushika wadhifa huo katika mabadiliko madogo ya Baraza la
Mawaziri yaliyompeleka aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Mwigulu Nchemba
kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri Tizeba alisema wakati ambapo tathmini ya chakula nchini ikiwa
haijakamilika, Kurugenzi ya Usalama wa Chakula imekuwa ikitoa vibali vya
chakula kusafirishwa nje ya nchi, huku ikiwa haijulikani kama chakula
kilicho kinatosha au hakitoshi na ili ziada ilindwe.
“Mbali ya kwamba hali ya chakula nchini ni nzuri lakini kumekuwepo na
wimbi la wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi wakipewa vibali na
kununua mazao ndani ya nchi na kuyauza nje ilhali tathmini ikiwa
haijakamilika,” alisema Tizeba.
Alitoa wiki mbili kuanzia sasa ukaguzi wa chakula nchini uwe
umefanyika ili kupatikana kwa tathmini halisi katika kipindi cha mwaka
2015/2016 kwani ununuzi wa mazao hayo umeonekana mkubwa na hali hiyo
isipodhibitiwa hali itakuwa mbaya zaidi.
Alisema vibali hivyo vimekuwa vikitolewa kinyume cha utaratibu kwa
kuwa tathimini ilitakiwa kufanyika kwanza, hivyo Katibu Mkuu amsimamishe
kazi mkurugenzi huyo na uchunguzi ufanyike dhidi yake pamoja na vibali
ambavyo vimekuwa vikitolewa tangu mwaka jana kwani havina harufu nzuri.
“Hata hivi karibuni nimepata taarifa kuna mfanyabiashara kapewa
kibali cha kusafirisha tani laki tatu kupeleka nchini Malawi, mfanye
uchunguzi wa vibali vyote alivyovitoa,” alisema Tizeba.
Kuhusu NFRA, Dk Tizeba alisema umekuwepo udhaifu mkubwa katika ghala
la Songea, Dodoma na Sumbawanga ambako mazao yameharibika na kusababisha
hasara huku uongozi wa wakala licha ya kuombwa vibali vya kununuliwa
kwa mazao hayo kama chakula cha mifugo havikutolewa.
Akizungumzia uvuvi bahari kuu, ameiagiza Kurugenzi wa Uvuvi
kubadilisha masharti ya leseni ya uvuvi katika bahari kuu ili kuangalia
uwezekano wa kufanya ubia na wavuvi hao ili Watanzania nao waweze
kunufaika na mavuno ya mazao hayo.
Alisema kwa wale ambao wana leseni hazitofanyiwa mabadiliko lakini kwa zile mpya na sheria haizuii kufanya hivyo.
Alisema hivi sasa zipo meli 105 zote zikitoka nje ya nchi zikiwa
zinaendelea na uvuvi na kuchota chochote na kuondoka, huku mamlaka ya
bahari wakiwa wanayajua hayo, wakidai kuwa Tanzania haina mahali pa
kushushia.
Alisema kuanzia sasa meli zote ziambiwe mazao yote watakayovuna
ambayo ni tofauti na leseni zao zinavyotaka yaletwe Dar es Salaam,
yagawiwe kama itakavyohitajika kwani Tanzania imeendelea kuwa shamba la
bibi kutokana na kukosa uwezo wa kuvua katika bahari kuu.
No comments:
Post a Comment