WAKAZI wa Dodoma jana asubuhi waliingiwa na taharuki baada ya mji huo
kukumbwa na tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa kipimo cha Richter 5.1.
Akizungumza jana ofisini kwake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia
Tanzania, Profesa Abdulkarim Mruma alisema tetemeko hilo lililotokea saa
12.01:15 asubuhi wakati wananchi wengi wakiwa wamelala na ni kubwa
ukilinganisha na matetemeko ambayo yamezoeleka kutokea yenye ukubwa wa
Richter 3.
Profesa Mruma alisema kitovu cha tetemeko hilo kilikuwa katika Bonde la Haneti - Itiso wilayani Chemba mkoani Dodoma.
Pia alisema kutokana na ukubwa wa tetemeko hilo, mikoa mingine ambayo
ipo karibu na eneo la chanzo cha tetemeko nayo imeathirika na kuitaja
mikoa hiyo iliyoathirika kuwa ni pamoja na Tanga, Dodoma, Singida upande
wa mashariki na Manyara.
Alisema tetemeko hutokea katika miamba migumu yenye madini ya
dhahabu. Akielezea chanzo cha tetemeko, Profesa Mruma alisema
limesababishwa na kupasuka kwa matabaka ya ardhi, na hutokea kutokana na
kuteleza kwa mapande hayo ambapo husababisha mtikisiko.
Alisema mapande ya ardhi ya Itiso ambayo yapo katika mtawanyiko wa
Bonde la Ufa la Arusha yanaendeleza kuteleza na kwamba tetemeko hilo ni
endelevu kwani bonde hilo la Itiso linazidi kusogea.
Alishauri watu wanaojenga maghorofa katika mkoa wa Dodoma kuzingatia
ushauri wa Wakala wa Jiolojia, kwani athari za kujenga majengo marefu
kwa mkoa huo bado zipo pale pale.
Aliwataka wanaojenga ghorofa waombe ushauri kwao kwani ukitaka kujenga ghorofa zaidi ya mbili ni lazima jengo liwe pana.
Kwa upande wa Mjiolojia Mwandamizi kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania
ambaye pia ni mtaalamu wa matetemeko, Gabriel Mbogoni alisema tetemeko
hilo limetokea maeneo ya Haneti kilometa 11 mashariki mwa mji wa Haneti
Wilaya ya Chemba ambao upo kilometa 79 kutoka kaskazini mashariki mwa
mji wa Dodoma.
“Hatujapata taarifa zozote za madhara labda kwa sababu bado ni mapema,” alisema Mbogoni.
No comments:
Post a Comment